Na Hadija Omary Mazezele-Tabora
Chama cha Msingi Mkombozi kilichopo Kata ya Tutuo Wilaya ya Sikonge kimezindua rasmi jengo jipya la ofisi litakalosaidia kuboresha huduma kwa wanachama na wakulima wa eneo hilo.
Jengo hilo lililogharimu zaidi ya shilingi milioni 165, likijumuisha gharama za ujenzi na ununuzi wa samani za ofisi, limeelezwa kuwa chachu ya kuimarisha utendaji na uwajibikaji ndani ya chama hicho.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Thomasi Myinga ambaye ndiye Mgeni Rasmi katika hafla hiyo amepongeza juhudi za chama hicho katika kujiimarisha kiutendaji na kiuchumi.
Aidha Myinga ameonya baadhi ya vyama vya ushirika vinavyoshindwa kusimamia maslahi ya wakulima ipasavyo, akisisitiza kuwa vyama vinapaswa kuwa nguzo ya maendeleo badala ya kuwa kikwazo.
Kwa upande wake Meneja wa Chama cha Msingi Mkombozi Mohamedi Sadick akaeleza katika Risala yake kuwa kuwa licha ya mafanikio hayo, bado wanakabiliwa na changamoto ya kupanda kwa bei za pembejeo, hali inayowaumiza wakulima na kupunguza tija ya uzalishaji.
Akijibu hoja hiyo, Mkuu wa Wilaya Myingaa amwsema kuwa suala la bei ya pembejeo tayari limefikishwa katika mamlaka husika, na kwamba baada ya majadiliano kukamilika, wananchi watapatiwa majibu na mwelekeo wa hatua zitakazochukuliwa.
Naye Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tabora, Venance Msafiri, akawataka viongozi wa vyama vya ushirika kuweka vipaumbele vinavyolenga maendeleo endelevu, uwazi na usimamizi bora wa rasilimali ili kukuza vyama vyao na kuongeza imani kwa wanachama.
Baadhi ya wanachama wa Chama cha Msingi Mkombozi Asha Mussa na Shabani Maulidi hawakuficha furaha yao kufuatia uzinduzi wa jengo hilo, wakisema kuwa ni ishara ya kukua na kuimarika kwa chama chao, huku wakitarajia kuona maboresho zaidi katika huduma na masoko ya mazao yao.
“Leo ni siku ya kihistoria kwetu wanachama wa Mkombozi Jengo hili ni ushahidi kuwa chama chetu kinakua na kinaelekea kwenye mafanikio makubwa,na tutajidhatiti kwenye uzalishaji Kwa manufaa yetu na kizazi Kijacho.alisemaAsha
Hata hivyo, uzinduzi wa jengo hilo jipya la Chama cha Msingi Mkombozi si tu mafanikio ya miundombinu bali ni hatua muhimu katika safari ya kuimarisha ushirika, uwajibikaji na ustawi wa wakulima wa Kata ya Tutuo na Wilaya ya Sikonge kwa ujumla.
Wakati chama kikionyesha mfano wa kujitegemea na kuwekeza katika maendeleo yake, changamoto ya kupanda kwa bei za pembejeo bado inahitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali na wadau wa sekta ya kilimo ili kulinda maslahi ya wakulima.
Hatua hiyo inaashiria matumaini mapya kwa wanachama, kwamba kupitia uongozi imara, uwazi na mipango endelevu, vyama vya ushirika vinaweza kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

















0 Comments