Dodoma.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno, amefunga rasmi mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali katika usimamizi na uendeshaji wa miradi ya Uwekezaji na Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public-Private Partnership – PPP).
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wakufunzi kutoka kampuni ya Cybiant ya nchini Malaysia, yamefungwa rasmi Februari 6, 2026 jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mhe. Maneno amesema kuwa lengo kuu la mafunzo ni kuwaongezea Mawakili wa Serikali uwezo na ujuzi katika mbinu za kisasa za majadiliano (negotiations), uchambuzi wa mikataba, ununuzi na utiaji saini wa mikataba, pamoja na usimamizi wake na upatikanaji wa taarifa muhimu za miradi mikubwa ya maendeleo.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo ni nyenzo muhimu kwa Mawakili wa Serikali katika kuhakikisha kuwa miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi inaleta tija na kulinda rasilimali za taifa.
“Mafunzo haya ni muhimu katika kujenga uwezo wa Mawakili wa Serikali ili kusimamia vyema mikataba ya PPP kwa maslahi mapana ya nchi,” amesema Maneno.
Aidha, amesisitiza kuwa mafunzo hayo yana mchango mkubwa katika kuhakikisha miradi ya PPP inaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Kupitia mafunzo haya tunaamini tutapata Mawakili wenye weledi na ubora mkubwa katika kuandaa na kusimamia mikataba ya miradi mikubwa, jambo litakalosaidia kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji kuelekea utekelezaji wa Dira 2050,” ameongeza.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Ildephonce Mukandara, kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, ameushukuru uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwezesha mafunzo hayo, akisema yamewasaidia kuongeza ujuzi katika upekuzi na usimamizi wa mikataba ya ubia, hivyo kuisaidia Serikali kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati endelevu wa Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa kuhakikisha watumishi wake wanaimarisha ujuzi na weledi unaohitajika katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

0 Comments