SERIKALI YAIMARISHA USHIRIKIANO NA SEKTA BINAFSI KUKUZA UCHUMI

 



Dar es Salaam


Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi pamoja na taasisi za fedha ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza uwekezaji nchini.


Akizungumza katika futari maalum iliyoandaliwa na Benki ya NBC kwa wateja wake katika Hoteli ya Rotana jijini Dar es Salaam, Balozi Omar amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika kujenga uchumi jumuishi na shindani unaochochewa na uzalishaji, uwekezaji na ubunifu wa kidijitali.


Balozi Omar amesema sekta ya fedha ina mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea viwanda, biashara na uwekezaji.


Aidha Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) kinaendelea kuhakikisha kinaratibu na kuimarisha ushirikiano huo ili kuvutia uwekezaji na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo.


Kwa upande wao, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw. Theobald Sabi, na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo, Dkt. Elirehema Doriye, wameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini, hali iliyochochea ukuaji wa sekta ya fedha na upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara.


Hafla hiyo ya futari iliwakutanisha viongozi wa Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na mshikamano katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.


#HatuaKwaHatua

@pppcentretanzania 






Post a Comment

0 Comments