DCEA YAKAMATA MAGUNIA 133 YA BANGI NA KUTEKETEZA HEKARI 68 MKOANI TABORA.
Na Hadija Omari Mazezele - Tabora.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imekamata magunia ya madawa ya kulevya aina ya bangi 133 yaliyokuwa yamefichwa ndani ya nyumba za watu na kuteketeza mashamba ya bangi hekari 68 zilizokuwa zimelimwa kwenye mapori ya msitu Wa hifadhi Igombe River uliopo wilaya uyui na pori la Nyahua lililopo wilayani sikonge mkoani Tabora.
Kamishina Jenerali wa (DCEA) Aretas Lyimo akitoa taarifa kwa waandishi wa habari hii leo Aprili 30, 2026 huko mjini Tabora amefafanua kwamba watuhumiwa saba wamekamatwa kufuatia oparesheni maalumu ya kuteketeza dawa za kulevya waliyoifanya kwa muda wa siku saba kwenye mapori hayo ya hifadhi kwa kushirikiana na wakala wa huduma za misitu (Tfs) kanda ya Magharibi.
Aidha mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya (DCEA) imeonya wananchi wanaoendelea kujihusisha na kilimo cha madawa hayo ya kulevya aina ya bangi huku ikisisitiza kwamba hakuna atakayebaki salama.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Tabora Paul Chacha ameiagiza TFS kuchukua hatua za haraka kwenye maeneo yote ya hifadhi mkoani humo ili kuhahkikisha wanatokomeza na kumaliza kabisa kilimo haramu cha madawa ya kulevya aina ya bangi.









0 Comments