AGENDA YAZINDUA MKAKATI WA KILIMO IKOLOJIA KUONDOA MATUMIZI YA VIUATILIFU HATARI KWA WAKULIMA

 


AGENDA YAZINDUA MKAKATI WA KILIMO IKOLOJIA KUONDOA MATUMIZI YA VIUATILIFU HATARI KWA WAKULIMA

Dar es Salaam, Mei 23, 2026 

Asasi isiyo ya kiserikali ya AGENDA imezindua mradi mpya wa kikanda unaolenga kuhamasisha wakulima wadogo kuachana na matumizi ya viuatilifu hatarishi sana (Highly Hazardous Pesticides – HHPs) na kuelekea katika matumizi ya mbinu za kilimo ikolojia (Agroecology), hatua inayotarajiwa kuongeza usalama wa chakula, kulinda afya za wakulima na kuhifadhi bioanuwai katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Uzinduzi wa mradi huo ulifanyika Mei 22, 2026 katika Hoteli ya Giraffe jijini Dar es Salaam, ukiwakutanisha wadau kutoka Tanzania, Kenya na Ethiopia katika warsha ya siku mbili iliyohitimishwa rasmi Mei 23, 2026.


Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Uthibiti kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel William Ndiyo, aliyemwakilisha Mkemia Mkuu wa Serikali. Akizungumza katika hafla hiyo amesema utekelezaji wa mradi huo utasaidia kuimarisha matumizi salama ya viuatilifu, kupunguza utegemezi wa kemikali hatarishi na hatimaye kuondoa matumizi ya viuatilifu vyenye athari kubwa kwa afya ya binadamu na mazingira.


Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda afya za wakulima, watumiaji wa mazao ya kilimo pamoja na vizazi vya sasa na vijavyo, huku ikiunga mkono juhudi za taifa katika kujenga mifumo endelevu ya uzalishaji wa chakula.


Kupitia mradi huo, zaidi ya wakulima 3,000 kutoka Tanzania, Kenya na Ethiopia wanatarajiwa kunufaika kupitia mafunzo ya kilimo ikolojia, uhamasishaji wa matumizi ya mbinu mbadala za kudhibiti visumbufu vya mazao pamoja na upatikanaji wa teknolojia salama za uzalishaji.


Mradi huo utalenga zaidi mazao ya pamba na mbogamboga, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakihusishwa na matumizi makubwa ya viuatilifu hatarishi katika uzalishaji wake.


Kwa upande wa Tanzania, mradi unaratibiwa na AGENDA kwa kushirikiana na Rainforest Alliance, huku ukijumuisha juhudi za kuwawezesha wakulima kupata vyeti vya kilimo hai (Organic Certification), hatua inayotarajiwa kuongeza thamani ya mazao, kuboresha ushindani wa bidhaa katika soko la ndani na kimataifa pamoja na kuongeza kipato kwa wakulima wadogo.


Wataalamu wa sekta ya kilimo wameeleza kuwa matumizi ya HHPs yameendelea kuchangiwa na ukosefu wa elimu ya kutosha, upatikanaji mdogo wa mbinu mbadala na utegemezi wa muda mrefu wa pembejeo za kemikali, hali ambayo imekuwa ikisababisha athari kwa afya ya binadamu, uchafuzi wa mazingira, kupungua kwa viumbe muhimu kama nyuki na kuathiri mfumo wa ikolojia.


Akizungumza wakati wa hitimisho la warsha hiyo ya kikanda, Afisa Programu Mkuu wa AGENDA, Silvani Mng’anya, amesema washiriki wamefikia maazimio muhimu yatakayokuwa msingi wa utekelezaji wa mradi katika nchi zote tatu.


Maazimio hayo ni pamoja na kuimarisha elimu na uhamasishaji kwa wakulima kuhusu madhara ya viuatilifu hatarishi na faida za kilimo ikolojia; kuanzisha na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta za kilimo, afya, mazingira na taasisi za utafiti; kuharakisha upatikanaji wa mbinu mbadala salama za kudhibiti wadudu na magonjwa ya mazao; pamoja na kuimarisha mifumo ya sera na usimamizi ili kupunguza matumizi ya HHPs katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Aidha, warsha hiyo imeazimia kuundwa kwa kamati za kitaifa za ushauri wa kiufundi katika kila nchi zitakazoratibu utekelezaji wa shughuli za mradi, kufuatilia maendeleo na kusaidia uhamishaji wa maarifa kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo.


Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Wizara ya Kilimo, Afisa Maendeleo ya Jamii Heremia Herman, amesema mradi huo utakuwa chachu ya kuongeza uelewa kwa wakulima kuhusu mbinu rafiki za uzalishaji ambazo zinalinda afya ya binadamu huku zikihifadhi mazingira.


Naye Afisa Programu wa Rainforest Alliance kutoka Kenya, Fredrick Otieno, amesema changamoto ya matumizi ya viuatilifu hatarishi si ya Tanzania, Kenya au Ethiopia pekee, bali ni suala la kimataifa linalohitaji ushirikiano mpana kati ya sekta za kilimo, afya, mazingira na wadau wa maendeleo.


Mradi huo unatekelezwa na AGENDA Tanzania kwa kushirikiana na PAN Ethiopia, CEJAD Kenya, PAN International pamoja na Rainforest Alliance, na unafadhiliwa na Global Framework on Chemicals Fund (GFC Fund) chini ya United Nations Environment Programme (UNEP).


Kupitia utekelezaji wake, mradi unatarajiwa kuwa sehemu ya mabadiliko ya muda mrefu katika sekta ya kilimo kwa kuhamasisha uzalishaji unaolinda afya ya binadamu, kuhifadhi bioanuwai, kuongeza ustahimilivu wa mifumo ya chakula na kujenga kilimo endelevu kwa wakulima wadogo wa Afrika Mashariki.
















Post a Comment

0 Comments