Na Hadija Omary Mazezele
Baadhi ya wakulima wa kata ya
Ndevelwa, Manispaa ya Tabora, wamezitaka mamlaka husika na wadau wa maendeleo
kuhakikisha ahadi zilizotolewa katika Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya
Tabianchi (COP30) zitekelezwe kwa vitendo ili kuwanufaisha wakulima, hususani
katika miradi ya mabwawa ya maji, upatikanaji wa pembejeo na nyenzo za kisasa
za kilimo.
Wakulima hao wamesema kuwa licha ya
kuwepo kwa ahadi nyingi zinazolenga kuwasaidia wakulima kukabiliana na athari
za mabadiliko ya tabianchi, utekelezaji wake bado haujaonekana kikamilifu
katika ngazi ya jamii.
Miongoni mwa wakulima waliotoa maoni
yao ni Halima Musa, Juma Magodi na Hamisi Raulence, wakulima wa kata ya
Ndevelwa, ambao wamesema kuwa utekelezaji wa ahadi za COP30 ni muhimu kwa
ustawi wa kilimo na maisha ya wakulima wadogo.
Halima Musa alisema kuwa mabadiliko
ya tabianchi yameendelea kuathiri uzalishaji wa kilimo, huku wakulima wakikosa
miundombinu ya uhakika ya maji kama mabwawa ya kuvunia maji ya mvua, jambo
linalofanya kilimo kutegemea mvua zisizotabirika.
“Ahadi zinazotolewa kwenye mikutano
ya kimataifa kama COP30 zinapaswa kushuka hadi ngazi ya mkulima. Tunahitaji
kuona mabwawa yanajengwa na miradi ya maji ikitekelezwa ili tuweze kulima kwa
uhakika,” alisema Halima.
Kwa upande wake, Juma Magodi alisema
kuwa upatikanaji wa pembejeo bora na kwa wakati ni changamoto kubwa kwa
wakulima wa Ndevelwa, huku akisisitiza kuwa ahadi za kusaidia wakulima wadogo
zinapaswa kutafsiriwa kwa vitendo.
“Tunaposikia kuna fedha na mipango
ya kusaidia wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, tunatarajia kuona
pembejeo, mbegu bora na nyenzo za kilimo zikifikishwa kwa wakulima, si kubaki
kwenye makaratasi,” alisema Juma.
Naye Hamisi Raulence alisema kuwa
uwajibikaji katika utekelezaji wa ahadi za COP30 ni jambo la msingi,
akibainisha kuwa bila ufuatiliaji na utekelezaji thabiti, wakulima wataendelea
kuwa waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi.
Wakulima hao wamezitaka serikali, wadau
wa maendeleo na taasisi zinazohusika na masuala ya mabadiliko ya tabianchi
kuhakikisha kuwa ahadi zinazotolewa katika mikutano ya kimataifa kama COP30
zinapangwa, kufuatiliwa na kutekelezwa kwa uwazi ili kuleta mabadiliko halisi
katika maisha ya wakulima.

0 Comments