WAKULIMA WA TABORA WAELEWA UMUHIMU WA COP30, WAJIPANGA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI.

 


Na Hadija Omary Mazezele

Wakulima mkoani Tabora wameonesha uelewa mzuri kuhusu maana na umuhimu wa Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP30, wakisema kuwa uelewa huo utawasaidia kufuatilia kwa karibu mikutano ijayo ya COP ili kunufaika na huduma za hali ya hewa pamoja na ajenda zitakazojadiliwa.

Miongoni mwa wakulima waliopata uelewa huo ni Kidumila Mtandi, Asha Salumu na Joseph Wilson, wakulima kutoka kijiji cha Chang’ombe, wilaya ya Tabora ambao walifuatilia mkutano wa COP30 na kuelewa kwa kina masuala yaliyojadiliwa.

Wakulima hao walisema kuwa kupitia ufuatiliaji wa COP30, wamepata ufahamu kuhusu namna dunia inavyojadili mabadiliko ya tabianchi, athari zake kwa kilimo, pamoja na hatua zinazochukuliwa kuboresha upatikanaji wa huduma za hali ya hewa kwa wakulima wadogo.

“Nimeelewa kuwa mikutano ya COP inajadili mambo yanayotugusa moja kwa moja kama wakulima, ikiwemo taarifa za hali ya hewa, mbinu za kukabiliana na ukame na mvua zisizotabirika,” alisema Kidumila Mtandi.

Kwa upande wake, Asha Salumu alisema kuwa uelewa wa COP30 umemsaidia kujua umuhimu wa kufuatilia mikutano ijayo ili kupata taarifa zitakazosaidia kupanga shughuli za kilimo kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Naye Joseph Wilson alisema kuwa maarifa waliyoyapata yatawasaidia kuelewa vyema kile kinachozungumzwa katika mikutano ijayo ya COP, hususan masuala yanayohusu huduma za hali ya hewa, teknolojia rafiki kwa mazingira na fursa za kuwawezesha wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Wakulima hao wamesema kuwa kufuatilia mijadala ya COP kutawasaidia kuongeza uzalishaji, kupunguza hasara zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, na kushiriki kikamilifu katika jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika jamii zao.

Post a Comment

0 Comments