TABORA.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jacobs Mwambegele, amewataka watendaji wa uchaguzi kuheshimu viapo vyao na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Katiba, sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi.
Jaji Mwambegele ametoa wito huo leo, Septemba 29, 2026, mkoani Tabora wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi yanayolenga kuwaandaa kwa uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Chamwino, Mkoa wa Dodoma, pamoja na uchaguzi wa madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara ambapo Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Novemba 4, 2026.
“Ninawasisitiza kuheshimu viapo vyenu kwa nafasi mlizoteuliwa, tekelezeni majukumu yenu kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, kanuni za maadili ya uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na yatakayotolewa na Tume katika kipindi hiki cha uchaguzi,” amesema Jaji Mwambegele.
Amewataka watendaji hao kuhakikisha kuwa katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi, wanavishirikisha kwa karibu vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili pamoja na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yao, hususan katika masuala wanayostahili kushirikishwa.
Aidha, amewaelekeza kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia kura ili kuviwezesha kupanga mawakala wao kwa wakati.
Jaji Mwambegele pia amewataka watendaji hao kuyatambua na kuyafahamu vizuri maeneo ambayo uchaguzi utafanyika, ikiwemo miundombinu ya kufika katika vituo vya kupigia kura.
“Ni muhimu kwenu pia kuhakikisha mnayatambua na kuyajua vyema maeneo ambayo uchaguzi utaendeshwa, ikiwemo miundombinu ya kufika katika vituo vya kupigia kura,” amesema.
Amesisitiza kuwa watendaji hao wanapaswa kuepuka kufanya kazi kwa mazoea, licha ya baadhi yao kuwa na uzoefu katika uendeshaji wa uchaguzi, akieleza kuwa kila uchaguzi una mazingira na mahitaji yake.
Vilevile, amewataka kuhakikisha kuwa watendaji wa vituo wanaoajiriwa wanakuwa na sifa, weledi na uadilifu unaohitajika, huku akiwataka kuachana na upendeleo wa kuwateua ndugu na jamaa wasio na sifa.
Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele amewataka watendaji kuhakiki vifaa vya uchaguzi wanavyovipokea kutoka Tume na kuhakikisha kila mkuu wa kituo anapatiwa vifaa vyote vinavyohitajika kwa wakati.
Aidha amewataka kuweka utaratibu utakaowezesha vituo vyote vya kupigia kura kufunguliwa saa 1:00 asubuhi siku ya uchaguzi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanawahusisha Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ununuzi na Wahasibu.
Kata 11 zitakazofanya uchaguzi wa udiwani ni Nonde katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya; Lugenge katika Halmashauri ya Mji Njombe; Bargish katika Halmashauri ya Mji Mbulu; Makole katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza; Mwera katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na Oldonyosambu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Kata nyingine ni Igalula katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui; Shelui katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba; Mvumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa; Nyarero katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Ilolangulu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.




0 Comments