BIMA YA AFYA KWA WOTE: TABORA YATAKA HUDUMA BORA NA LUGHA NJEMA KWA WAGONJWA

 





NA HADIJA OMARI MAZEZELE, TABORA

Serikali mkoani Tabora imewataka waganga wa wilaya na watoa huduma za afya kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vinakuwa na mazingira rafiki kwa watumiaji wa Bima ya Afya kwa Wote, huku ikisisitiza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba pamoja na matumizi ya lugha nzuri kwa wagonjwa.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Dkt. Gerald Mongella, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Beno Malisa, wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya Bima ya Afya kwa Wote mkoani Tabora.


Dkt. Mongella amesema ubora wa huduma za afya hauishii katika upatikanaji wa matibabu pekee, bali unahusisha pia namna wagonjwa wanavyopokelewa, wanavyohudumiwa na wanavyoheshimiwa wanapofika katika vituo vya afya.


Amesisitiza kuwa matumizi ya lugha mbovu yanaweza kuongeza maumivu ya kisaikolojia kwa wagonjwa ambao tayari wanakabiliwa na changamoto za kiafya, hivyo kuwataka watumishi wa afya kuzingatia lugha ya staha, huruma na heshima kwa kila mgonjwa bila kujali aina ya malipo au bima anayotumia.


“Unakuta mgonjwa anafika hospitalini tayari ana trauma ya ugonjwa, halafu unakwenda kumuongezea trauma nyingine kwa lugha mbovu. Kwa hili, maelekezo yangu ni kwamba hatua zichukuliwe,” amesema Dkt. Mongella.


Aidha, amewataka waganga wa wilaya, chini ya usimamizi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa wakati, pamoja na kupanga vizuri watumishi ili kuboresha utoaji wa huduma katika maeneo yote.


Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, amesema awamu ya pili ya Bima ya Afya kwa Wote inatarajiwa kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi na kuwawezesha kupata huduma za afya kwa urahisi zaidi.





Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiunga na mpango huo ili kuongeza uhakika wa upatikanaji wa huduma za matibabu wanapozihitaji.


Naye Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Tabora, Dkt. Raphael Mallaba, ametoa wito kwa viongozi wa ngazi zote kushirikiana katika kuhakikisha taarifa za walengwa zinathibitishwa kwa wakati ili kurahisisha utekelezaji wa mpango huo.


Baadhi ya wananchi waliojitokeza kujiunga na mpango huo wameishukuru Serikali kwa kuanzisha Bima ya Afya kwa Wote, wakieleza kuwa awali walikabiliwa na changamoto ya kupata huduma za matibabu kwa wakati kutokana na kushindwa kumudu gharama zake.


Wamesema mpango huo unatoa fursa ya kupata huduma za afya kwa urahisi zaidi na kupunguza hofu ya gharama wanapougua.


Uzinduzi wa awamu ya pili ya Bima ya Afya kwa Wote ni sehemu ya juhudi za kupanua upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi. Hata hivyo, utekelezaji wenye tija unahitaji ushirikiano wa wananchi, viongozi na watoa huduma za afya, pamoja na kuhakikisha dawa, vifaa tiba na huduma zinazozingatia utu wa mgonjwa vinapatikana kwa wakati.









Post a Comment

0 Comments