TABORA
Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Mhe. Sauda Mtondoo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Beno Malisa, ameongoza kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka 2025/26, akizitaka Halmashauri kuimarisha afua za lishe, afya na usafi wa mazingira. Kikao hicho, kilichowakutanisha wajumbe na wadau wa lishe, kimefanyika Oktoba 9, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Mtemi Isike Mwanakiyungi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Awali, akitoa neno la utangulizi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, amepongeza Halmashauri kwa kufanya vizuri katika utekelezaji wa viashiria vya Mkataba wa Lishe, hususan utoaji wa shilingi 1,000 kwa kila mtoto, kwa kuzingatia idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika Halmashauri husika.
Akizungumza na wajumbe, Mhe. Mtondoo amezitaka Halmashauri kuhamasisha wasindikaji wa unga wa mahindi kuongeza virutubishi kwenye unga na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuutumia. Aidha, ameelekeza Halmashauri kujumuisha katika mipango yao mahitaji halisi ya wataalamu wa afya ya mazingira na kushirikisha wadau katika utekelezaji wa afua za kinga na kuzuia milipuko ya magonjwa.
Katika kuimarisha malezi na ulinzi wa watoto, amewataka Wakurugenzi kuanzisha vituo vya kijamii vya kulelea watoto mchana, hususan maeneo ya masoko, ili watoto wa wazazi wanaofanya biashara wapate malezi bora, lishe na ulinzi katika mazingira salama. Pia, ameelekeza kuchukuliwa kwa hatua stahiki kwa wazazi au walezi wanaowaruhusu watoto kurejea mitaani baada ya kuondolewa na kuunganishwa na familia zao.
Mhe. Mtondoo ametoa miezi mitatu kwa kila Halmashauri kuhuisha sheria ndogo zinazohusu afya, lishe na mazingira, pamoja na kuhuisha na kuzijengea uwezo kamati za afya na mazingira katika ngazi za kata, mitaa na vijiji. Amesisitiza pia kutekelezwa kwa zoezi la usafi jumuishi na shirikishi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, huku kila Halmashauri ikiwa na mratibu anayetambulika na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji ofisi ya Mkuu wa mkoa kila ifikapo mwisho wa mwezi.














0 Comments