NA HADIJA OMARI MAZEZELE,TABORA
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Tabora unatarajia kuzindua awamu ya pili ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kesho, Oktoba 22, 2026, hatua inayolenga kupanua wigo wa wananchi wanaopata huduma za afya kupitia bima.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa NHIF Mkoa wa Tabora, Dkt. Raphael Francis Malaba, amesema awamu hiyo ya pili itahusisha vikundi, watu binafsi na kaya zenye idadi ya watu wasiozidi sita, kufuatia kukamilika kwa awamu ya kwanza iliyolenga kaya maskini.
Dkt. Malaba amesema utekelezaji wa awamu hiyo unaenda sambamba na bajeti ya Serikali ya zaidi ya shilingi bilioni 93.814 katika mwaka huu wa fedha, fedha zilizotengwa kwa ajili ya kugharamia matibabu ya kaya maskini 625,000 kote nchini kupitia Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Amesema mpango huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kupanua upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kufahamu utaratibu wa kujiunga na kunufaika na huduma zinazotolewa chini ya mpango huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, John Mongela, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo utakaofanyika katika viwanja vya TBC, Manispaa ya Tabora.
Mongela amesema uzinduzi huo utatoa fursa kwa wananchi kupata taarifa kuhusu mpango huo na kujiandikisha ili kunufaika na huduma za afya kupitia utaratibu wa bima.
Aidha, amewasisitiza wananchi kutumia fursa hiyo kujiunga na bima ya afya, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuwawezesha kupata huduma za matibabu kwa utaratibu unaotambuliwa na mpango huo.
Uzinduzi wa awamu ya pili unatarajiwa kuwa sehemu ya hatua za kupanua wigo wa wananchi wanaoweza kunufaika na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote nchini.






0 Comments